Today's Date:28-06-2017
 
  A Monthly Newsletter of SJUT
  Newsletter, Volume 1 Issue 2
  Newsletter, Volume 1 Issue 1
   
  Other website Links
  Admission criteria
  Fee structure
  SJUT Prospectus
  SJUT Annual Calendar
  Lecture Timetable
  Quality Assurance
  • Science society
  SJUT Chapel
  SJUT Dress Code
  SJUT Library
  SJUT Policies and Forms
  Examination Results
  E-Learning
  Previous announcements
  Our Centres
    •  St.Mark's Centre
    •  Msalato Theological College
    •  Town Centre- Dodoma
Journals and website links
    • TCU
    • HESLB
    • The Anglican Church of Tanzania
    • Soma Journal
    • AJTS
Webmail & Social Madia
 

 

 

HOTUBA YA MAKAMU MKUU WA CHUO
REV PROF EMMANUEL D MBENNAH
KATIKA MAHAFALI YA SITA YA
ST JOHN’S UNIVERSITY OF TANZANIA
MAZENGO, DODOMA
5 DESEMBA 2015

Hotuba katika PDF

 • Mhashamu Baba Askofu Mkuu, the Most Rev Dr Jacob Erasto Chimeledya, Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania, Askofu wa Dayosisi ya Mpwapwa, na Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa St John’s University of Tanzania,
 • Mheshimiwa Mkuu wa Chuo, Baba Askofu Mkuu Mstaafu Donald Leo Mtetemela,
 • Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Kanali Mstaafu Chiku Galawa,
 • Baba Maaskofu, Wadhamini wa Chuo Kikuu cha St John’s University of Tanzania,
 • Mheshimiwa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu, Balozi Paul Rupia,
 • Wajumbe wa Baraza la Chuo,
 • Waheshimiwa Mabalozi,
 • Viongozi wa Serikali, Vyama vya Siasa, Madhehebu ya Dini na Asasi za Kiraia
 • Makamu Mkuu wa Chuo wa Kwanza Prof Manoris Meshack
 • Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, Taaluma, Prof Casmir Rubagumya,
 • Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, Mipango, Fedha na Utawala, Prof Yohana Msanjila,
 • Wageni Waalikwa,
 • Wanajumuia wa St John’s University of Tanzania,
 • Wahitimu,
 • Mabibi na Mabwana,

   Bwana Yesu asifiwe.

Mheshimiwa Mkuu wa Chuo,
Katika mahafali haya ya Sita ya St John’s University of Tanzania nimeona nizungumzie, kwa kifupi, mambo matatu.

Lakini kwanza nikukaribishe wewe, Mheshimiwa Mkuu wa Chuo, niwakaribishe Baba Maaskofu, na kipekee Baba Maaskofu Wastaafu na wake zao. Wengi wenu Baba Wastaafu, ndio mliopokea na kuyatekeleza maono ya kuanzisha Chuo Kikuu hiki, wakati huo mkiwa kazini.

Aidha niwakaribisheni wazazi, wenzi, watoto, waajiri na waajiiri watarajiwa, wafadhili, na ndugu na jamaa wa karibu wa wahitimu wetu.

Na kwa wageni wetu waalikwa wengine, na wote mliofika kushiriki na kushuhudia siku hii muhimu, napenda kuwakaribisheni sana.

Baada ya maneno hayo ya ukaribisho, niseme mambo matatu.

1. SHUKRANI
Kwanza, Mheshimiwa Mkuu wa Chuo, ni neno la shukrani.

Mungu kwa neema na upendo wake ametujalia mafanikio kadhaa ya msingi. Nitaje mambo machache kuwakilisha mengi ambayo Mungu alitujalia kufanikisha katika mwaka wa masomo uliopita:

 • Tulifanikiwa kupata Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, wa Mipango, Fedha na Utawala, Prof Yohana Petro Msanjila, aliyejiunga nasi tarehe 1 Machi 2015.
 • Wakuu wa vitivo na skuli, na wakurugenzi wa idara za taaluma kadhaa wapya waliteuliwa, na kwa kufanya hivyo tulifanikiwa kuondoa nafasi nyingi za ukaimu, hali ambayo imetuwezesha kuimarisha zaidi utendaji na usimamizi na uendeshaji vitengo vya taaluma.
 • Jitihada zetu za kuongeza miundombinu ziliendelea. Katika hili, tulifanikiwa kukamilisha michoro na Mipango Biashara (Business Plans) kwa ajili ujenzi wa hosteli, ikiwa ni sehemu ya dhamira yetu kuongeza nafasi za malazi kwa wanafunzi 2,200, na pia kwa ajili ya jengo jipya la utawala kwa ajili ya ofisi za kutosha watumishi 90. Mawasiliano na wadau mbalimbali yanaendelea kwa ajili ya kupata fedha zinazohitajika ili kuanza ujenzi.
 • Watumishi wetu wanne walimaliza masomo yao ya shahada za uzamivu, zote zikiwa ni PhDs (1 USA, 2 New Zealand, na 1 Afrika Kusini), jambo ambalo limeongeza nguvu yetu ya kufundisha na kusimamia utafiti.
 • Tulianzisha kozi mpya zaidi ya 11 za astashahada na stashahada, zikiwemo stashahada ya Elimu kwa shule za msingi na stashahada ya Elimu ya Sayansi.
 • Chuo kilifanya mkutano wa kwanza wa utafiti, ambapo watafiti mbalimbali kutoka ndani na nje ya St John’s University, wakiwemo baadhi yao kutoka Marekani na Ujerumani, walizungumzia tafiti wanazofanya. Na kwa mkutano huo pia Chuo kilizindua utaratibu ambao tutaufanya kila mwaka.

Tunamtukuza Mungu kwa kutujalia imani, uvumilivu na mshikamano.

Mheshimiwa Mkuu wa Chuo, napenda pia niwashukuru kwa dhati wahadhiri wote wa St John’s University, Manaibu Makamu Mkuu wa Chuo, wakuu wa vitivo na skuli, na watumishi wenginge wote wa St John’s University katika idara na vitengo mbalimbali. Kwa umahiri wao na bidii yao, wamefanikisha maandalizi mazuri ya wahitimu wetu leo.

Mheshimiwa Mkuu wa Chuo, napenda nitumie fursa hii kuungana na Watanzania wengine kumshukuru Mungu kwa kutujalia kumaliza Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani salama na kwa amani. Na zaidi, kumshukuru Mungu kwa kutupatia Rais ambaye katika kipindi kifupi ameonesha moyo wa dhati wa kuipenda nchi yetu, kuwapenda Watanzania, na dhamira thabiti ya kupambana na rushwa, ufisadi, na ukosefu wa uadilifu katika utumishi. Kwa niaba ya Jumuiya ya St John’s University of Tanzania napenda kuwapongeza viongozi wetu hawa wapya: Mheshimiwa Dr John Magufuli kwa kuchaguliwa kwake kuiongoza nchi yetu katika msimu huu: Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa kuchaguliwa kwake Makamu wa Rais; na Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa, kwa kuteuliwa kwake kuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tano. Hapana shaka Watanzania tutatambua kuwa huu ni musimu wa kurejesha heshima, uadilifu, na uaminifu katika kazi kwa ujumla.

Pamoja na pongezi hizo kwa viongozi wetu hawa wa kitaifa, pia niwashukuru serikali mkoani Dodoma, tukianzia na Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa; Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi (MoEVT); Tume ya Vyuo Vikuu (TCU); Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE); na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB). Hawa wote, kwa namna mbalimbali, wametupa ushirikiano kadiri tulivyohitaji.

Hilo ni jambo la kwanza. Neno la shukrani.

2. BAADHI YA MIPANGO NA MALENGO YA CHUO KIKUU

Pili, Mheshimiwa Mkuu wa Chuo,

Katika mwaka wa masomo uliopita Chuo kilipita katika changamoto kadhaa nzito zilizotokana na mtiririko wa historia yetu kama chuo kikuu. Baadhi ya changamoto hizi bado zipo, hususan, uhitaji wa kuimarisha na kupanua miundombinu, na kuimarisha hali ya chuo kifedha ili kuboresha huduma kwa wadao wote wa chuo.

Nipende kuwashirikisha baadhi ya mipango yetu ya mbeleni kama Chuo Kikuu, kwa ajili ya sala zenu na ushiriki wenu wa hali na mali:
Utume wetu ni ule ule. Kuwa kituo bora cha kumwendeleza mwanadamu katika ujumla wa maisha yake kujifunza kutumika.

Na maono yetu ya St John’s University of Tanzania ya wakati ujao ni yale yale: Kuwa chuo kikuu cha Kikristo chenye ubora wa kushindana kimataifa na ambacho ni chanzo cha mafafanuzi ya viwango kwa zile taaluma tutakazokuwa tumejikita.

Katika kuelekea huko, tunaendelea kuimarisha uelewa wa maono yetu haya, na uadilifu katika maeneo yote ya utendaji wetu. Tunazidi kuimarisha utamaduni wetu wa kutoa elimu ya chuo kikuu bora kabisa, kwa manufaa ya wahitimu, na kwa taifa kwa ujumla, na kwa sifa na utukufu wa Mungu.

Katika dhamira yetu ya kuzidi kuimarisha Chuo, tunaendelea na utekelezaji wa mipango yetu ya kuongeza na kuboresha miundombinu: Hii ni pamoja na nafasi za kulala wanafunzi, ofisi za walimu, nyumba za watumishi, jengo la utawala zikiwemo ofisi kwa ajili ya watumishi hasa wahadhiri, ukumbi wa mikutano, na kuimarisha teknolojia ya mawasiliano. Sambamba na hayo, tutaendelea kuanzisha kozi mpya kwa ngazi mbalimbali, zikiwemo shahada za uzamivu, yaani PhDs. Nichukue fursa hii kuwaalika wawekezaji na wahisani kuungana nasi ili kufanikisha mipango hii.

Lakini pia, Chuo kimeandaa mpango wa kushirikisha Waanglikana wa Tanzania na Watanzania wengine wenye mapenzi na Chuo kwa kuwatia moyo kuchangia fedha kwa ajili ya kuimarisha uendeshaji wa Chuo na kutekeleza mipango ya maendeleo ya Chuo. Mpango huu unatekelezwa kwa kushirikiana na baadhi ya Dayosisi za Kanisa Anglikana Tanzania.

3. NENO KWA WAHITIMU

Na tatu, Mheshimiwa Mkuu wa Chuo,

Niwapongeze wahitimu wetu wa leo na kutoa wito wangu kwa Watanzania. Na sasa kwenu wahitimu: Mmefanya kazi kwa bidii. Mmefika hatua mbalimbali za kitaaluma. Ni matumaini yangu kuwa siyo tu mmepitia elimu ya chuo kikuu, hapa St John’s University, lakini pia kwamba elimu ya chuo kikuu imewapitia ninyi. Ni imani yangu ya daima, kwamba mtu anayesoma chuo kikuu asiishie kupata uwezo, ujuzi na upeo ambavyo haikuwa lazima kuja chuo kikuu kuvipata.

Mheshimiwa Mkuu wa Chuo, niwakumbushe wahitimu wetu wa leo, kwamba St John’s University of Tanzania ina dhana ya aina ya mhItimu tunayetaka kutayarisha. Huyu mtu aliyeendelezwa katika ujumla wa maisha yake na kuwa amejifunza kutumika anatambulikaje?

 • Zaidi ya yote, ni mhitimu wenye hofu ya Mungu.
 • Ni mhitimu aliyetayarishwa kikamilifu katika taaluma yake, kwa hiyo ana ujuzi, uelewa na uwezo wa viwango sawasawa na mahali popote duniani kwa fani hiyo na ngazi aliyosoma, na kwa hiyo ni mwenye uwezo wa kufanya kazi mahali popote.
 • Ni mhitimu mwenye tabia ya kufikiri na kutafuta majawabu au ufumbuzi wa masuala.
 • Lakini pia ni mhitimu kiongozi na kiongozi mtumishi. Maana yake ni mwadilifu, mzalendo, mwenye upendo kwa wote, mwenye ujasiri na mwenye kujiamini.
 • Ni mhitimu mwenye maono na uchu wa jamii iliyobadilika na kuwa bora, na kwa tabia yake ni mhitimu mbunifu – innovative.
 • Ni mhitimu mwenye falsafa sahihi ya mafanikio na anayetambua kwamba kufanya kazi kwa bidii ni heshima ya pekee ambayo mwanadamu amepewa na Mungu.
 • Ni muhitimu anayeona uwezekano wa mabadiliko chanya na kufanya kila jitIhada kuchangia kuleta mabadiliko hayo.

Aidha, ni dhamira yetu kutayarisha mhitimu wa wakati ujao, graduate for the future. Tunaamini elimu ambayo mhitimu wetu anaipata inampa macho ya ziada, kuona ulimwengu unavyokwenda na unakokwenda, na kujua nafasi yake katika mtiririko huo.

Mheshimiwa Mkuu wa Chuo,

Kuna kisa tunachokisoma katika Injili, Bwana Yesu anawaona makutano wamechoka kama kondoo wasio na mchungaji. Katika kuwahurumia makutano, anawaambia Wanafunzi wake kwamba mavuno ni mengi bali watendakazi ni wachache. Wazo hili la uchache ni wazo pana. Kwa maana ya kisa chenyewe, yawezekana uchache unaozungumziwa ni uchache wa idadi - idadi ya watu wanaohitajika kuifanya ile kazi vizuri ni ndogo. Lakini kuna vipengele vingine vya uchache: Uchache wa nia, uchache wa dhamira, uchache kwa maana ya viwango, na uchache katika mtawanyiko.

Nchi yetu ina uchache. Kwa mujibu wa takwimu za 2008 za Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, nchi yetu ina wauguzi 3,280, ambapo idadi inayohitajika ilikuwa ni wauguzi 20,672. Hii ni miaka saba tu iliyopita. Sidhani hali imebadilika sana.

Vilevile, kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2008 za Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Tanzania ilikuwa na Wafamasia 640. Kwa sasa, kitaifa, kwa kila Watanzania milioni moja tuna Wafamasia 16 tu. Kimikoa, kwa Dar es Salaam, ni Wafamasia 137 kwa kila wakazi milioni moja, na kwa Mkoa wa Dodoma, kwa kila watu milioni moja tuna Wafamasia 10 tu. Ni uchache. Na hapa tunazungumzia uchache wa idadi tu.

Kwa upande wa walimu wa sekondari, takwimu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi za mwaka 2009, miaka sita tu iliyopita, nchi yetu ilikuwa na walimu wa sekondari 33,954, tuseme 34,000, ambayo ilikuwa ni kama 40% tu ya idadi iliyohitajika. Ni kweli miaka ya hivi karibuni serikali imetekeleza mikakati ya kuongeza idadi ya Walimu wa sekondari. Hata hivyo, pamoja na kupongeza juhudi hizo, siamini kwamba picha imebadilika sana. Bado kuna uchache, hata wa idadi tu.

Kwa upande mwingine, tukiangalia mwenendo wa ongezeko la idadi ya watu katika nchi yetu, tunaona kwamba mwaka 2022, miaka saba ijayo, idadi ya Watanzania itafikia 58,644,926, karibu milioni 59. Mwaka 2032, Watazania tutakuwa 76,548,181, ambapo mwaka 2042, tutakaribia kabisa kufikia milioni 100 (99,916,983). Ifikapo mwaka 2052, idadi yetu itafikia 130,419,866, karibu milioni 130.5. Na hii ni miaka 37 tu ijayo. Si mingi, na wengi wetu hapa tutakuwepo. Katika vipindi hivi vyote, Watanzania asilimia 68.5 watakuwa ni watoto na vijana chini ya umri wa miaka 30. Hii ni sawa na kusema, kwa kila Watanzania watatu, wawili watakuwa chini ya umri wa miaka 30.

Na katika kipindi cha miaka hii 37 ijayo, ulimwengu utafika mbali sana kisayansi, kiteknolojia, na kiubunifu. Inawezekana kabisa baadhi ya wanadamu watakuwa wamehamia sayari nyingine na kwenda kuishi huko. Inawezekana kabisa, tiba ya upasuaji kama tunavyozijua sasa kitakuwa ni kitu cha kihistoria. Inawezekana kabisa, tutakuwa katika uchumi usiotumia fedha. Usafiri wa anga utakuwa wa tofauti na wa kasi ya namna ambayo hatuwezi hata kupiga picha kwenye mawazo yetu kwa sasa. Inawezekana sana tutakuwa na magari yanayoweza kupaa. Kama Bwana alivyosema, Maarifa yataendelea kuongezeka sana.

Takwimu nilizozitaja zinaonesha kwamba tunayo fursa ya kubadili mwelekeo wa nchi yetu, maana tunaweza kuwekeza kwa watoto na vijana. Katika kufanya hivi, itapasa Tanzania ifikirie upya juu ya elimu tunayoitoa.

Tunaona kwa sasa tuna uchache wa idadi katika nyanja mbalimbali muhimu. Ni uchache wa idadi lakini pia kuna aina zingine zote za uchache. Pia ni dhahiri kwamba, kasi ya ongezeko la idadi ya watu nchini ni kubwa sana ukilinganisa na kasi ya kutayarisha watu watakaohitajika kutoa huduma muhimu.

Hata kwa upande wa Kanisa, ni muhimu kuangalia takwimu hizi na kutayarisha watu wa kutosha, kwa idadi na kwa aina, kwa ajili ya kuhudumia umma mkubwa na wa aina ya Watanzania watakaokuwepo.

Mheshimiwa Mkuu wa Chuo,
Leo ni siku njema, kwetu sisi St John’s University, kwa Kanisa, na kwa nchi yetu, ambapo wahitimu 1,741 watatunukiwa astashahada, stashahada, shahada, na shahada za uzamili katika fani mbalimbali.

Kwenu wahitimu wetu leo: Ni matumaini yangu kuwa mtakwenda kupunguza uchache wa aina zote. Mmepata elimu nzuri, na sasa mnakwenda kwenye uwanja wa kutumika. Nendeni mkawe mabalozi wazuri wa Chuo chenu, kwa utumishi wenu mahiri na kwa mwenendo wenu wa uadilifu. MMEJIFUNZA, SASA NENDENI MKATUMIKE.

Amen.

Prof Emmanuel D Mbennah, PhD, PhD
Makamu Mkuu wa Chuo

 

 
 
Copyright 2009 © St.John's University of Tanzania.Updated:Jun 2017 , All Rights Reserved.